Matayo 10
Swahili NT
1Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kutoa pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote.

2Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: wa kwanza ni Simoni aitwae Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake; 3Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtoza ushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo; 4Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

5Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: "Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika mji wa Wasamaria. 6Ila nendeni kwa watu wa Israeli waliopotea kama kondoo. 7Mnapokwenda hubirini hivi: Ufalme wa mbinguni umekaribia. 8Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo. Mmepewa bure, toeni bure. 9Msichukue mifukoni mwenu dhahabu, wala fedha, wala sarafu za shaba. 10Msichukue mkoba wa kuombea njiani, wala koti la ziada, wala viatu, wala fimbo. Maana mfanyakazi anastahili riziki yake. 11Mkiingia katika mji wowote au kijiji, tafuteni humo mtu yeyote aliye tayari kuwakaribisheni, na kaeni naye mpaka mtakapoondoka mahali hapo. 12Mnapoingia nyumbani wasalimuni wenyeji wake. 13Kama wenyeji wa nyumba hiyo wakiipokea salamu hiyo, basi, amani yenu itakaa pamoja nao. Lakini ikiwa hawaipokei, basi amani yenu itawarudia ninyi. 14Kama mtu yeyote atakataa kuwakaribisheni au kuwasikilizeni, basi mtokapo katika nyumba hiyo au mji huo, yakung'uteni mavumbi miguuni mwenu kama onyo kwao. 15Kweli nawaambieni, Siku ya hukumu mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile iliyoipata miji ya Sodoma na Gomora.

16Sasa, mimi nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa. 17Jihadharini na watu, maana watawapeleka ninyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao. 18Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kutangaza Habari Njema kwao na kwa mataifa. 19Basi, watakapowapeleka ninyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema. 20Maana si ninyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.

21Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua. 22Watu wote watawachukieni kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokolewa.

23Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.

24Mwanafunzi si mkuu kuliko mwalimu wake, wala mtumishi si mkuu kuliko bwana wake. 25Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mkubwa wa jamaa Beelzebuli, je hawatawaita watu wengine wa jamaa hiyo majina mabaya zaidi?

26Basi, msiwaogope watu hao. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, na kila kilichofichwa kitafichuliwa. 27Ninalowaambieni ninyi katika giza, lisemeni katika mwanga; na jambo mlilosikia likinong'onezwa, litangazeni hadharani. 28Msiwaogope wale wauao mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili pamoja na roho katika moto wa Jehanamu. 29Shomoro wawili huuzwa kwa senti tano. Lakini hata mmoja wao haanguki chini bila kibali cha Baba yenu. 30Lakini kwa upande wenu, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31Kwa hiyo msiogope; ninyi mu wa thamani kuliko shomoro wengi.

32Kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, mimi pia nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. 33Lakini yeyote atakayenikana hadharani, nami nitamkana mbele ya Baba yangu aliye mbinguni.

34Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35Maana nimekuja kuleta mafarakano kati ya mtu na baba yake, kati ya binti na mama yake, kati ya mkwe na mkwe wake. 36Na maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake.

37Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi, hanistahili. Ampendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. 38Mtu asiyechukua msalaba wake na kunifuata, hanistahili. 39Anayeyashikilia maisha yake, atayapoteza; lakini anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata.

40Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi, anamkaribisha yule aliyenituma. 41Anayemkaribisha nabii kwa sababu ni nabii, atapokea tuzo la nabii. Anayemkaribisha mtu mwema kwa sababu ni mtu mwema, atapokea tuzo la mtu mwema. 42Kweli nawaambieni, yeyote atakayempa mmojawapo wa wadogo hawa kikombe cha maji baridi kwa sababu ni mfuasi wangu, hatakosa kamwe kupata tuzo lake."



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 9
Top of Page
Top of Page