Swahili NT 1Wakati huo umati mkubwa wa watu ulikusanyika tena, na hawakuwa na chakula. Basi, Yesu akawaita wanafunzi wake, akawaambia,
2Nawahurumia watu hawa kwa sababu wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu, wala hawana chakula.
3Nikiwaacha waende nyumbani wakiwa na njaa watazimia njiani, maana baadhi yao wametoka mbali."
4Wanafunzi wake wakamwuliza, "Hapa nyikani itapatikana wapi mikate ya kuwashibisha watu hawa wote?"
5Yesu akawauliza, "Mnayo mikate mingapi?" Nao wakamjibu, "Saba."
6Basi, akawaamuru watu wakae chini. Akaitwaa ile mikate saba, akamshukuru Mungu, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu, nao wakawagawia.
7Walikuwa pia na visamaki vichache. Yesu akavibariki, akaamuru vigawiwe watu vilevile.
8Watu wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki yaliyosalia wakajaza makapu saba.
9Nao waliokula walikuwa watu wapatao elfu nne. Yesu akawaaga,
10na mara akapanda mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda wilaya ya Dalmanutha. 11Mafarisayo walikuja, wakaanza kujadiliana na Yesu. Kwa kumjaribu, wakamtaka awafanyie ishara kuonyesha anayo idhini kutoka mbinguni. 12Yesu akahuzunika rohoni, akasema, "Mbona kizazi hiki kinataka ishara? Kweli nawaambieni, kizazi hiki hakitapewa ishara yoyote!" 13Basi, akawaacha, akapanda tena mashua, akaanza safari kwenda ng'ambo ya pili ya ziwa. 14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate; walikuwa na mkate mmoja tu katika mashua. 15Yesu akawaonya, "Angalieni sana! Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode." 16Wanafunzi wakaanza kujadiliana wao kwa wao, "Anasema hivyo kwa kuwa hatuna mikate." 17Yesu alitambua hayo, akawaambia, "Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? Je, bado hamjafahamu, wala hamjaelewa? Je, mioyo yenu imeshupaa? 18Je, Mnayo macho na hamwoni? Mnayo masikio na hamsikii? Je, hamkumbuki 19wakati ule nilipoimega ile mikate mitano na kuwapa watu elfu tano? Mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki ya makombo?" Wakamjibu, "Kumi na viwili." 20Na nilipoimega ile mikate saba na kuwapa watu elfu nne, mlikusanya makapu mangapi ya makombo? Wakamjibu, "Saba." 21Basi, akawaambia, "Na bado hamjaelewa?" 22Yesu alifika Bethsaida pamoja na wanafunzi wake. Huko watu wakamletea kipofu mmoja, wakamwomba amguse. 23Yesu akamshika mkono huyo kipofu, akampeleka nje ya kijiji. Akamtemea mate machoni, akamwekea mikono, akamwuliza, "Je, unaweza kuona kitu?" 24Huyo kipofu akatazama, akasema, "Ninawaona watu wanaoonekana kama miti inayotembea." 25Kisha Yesu akamwekea tena mikono machoni, naye akakaza macho, uwezo wake wa kuona ukamrudia, akaona kila kitu sawasawa. 26Yesu akamwambia aende zake nyumbani na kumwamuru, "Usirudi kijijini!" 27Kisha Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika vijiji vya Kaisarea Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema mimi ni nani?" 28Wakamjibu, "Wengine wanasema wewe ni Yohane Mbatizaji, wengine Eliya na wengine mmojawapo wa manabii." 29Naye akawauliza, "Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?" Petro akamjibu, "Wewe ndiwe Kristo." 30Kisha Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake. 31Yesu alianza kuwafundisha wanafunzi wake: "Ni lazima Mwana wa Mtu apatwe na mateso mengi na kukataliwa na wazee na makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Atauawa na baada ya siku tatu atafufuka." 32Yesu aliwaambia jambo hilo waziwazi. Basi, Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea. 33Lakini Yesu akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro akisema, "Ondoka mbele yangu, Shetani! Fikira zako si za kimungu ila ni za kibinadamu!" 34Kisha akauita umati wa watu pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, "Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 35Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Habari Njema, atayaokoa. 36Je, kuna faida gani mtu kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake? 37Ama mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake? 38Mtu yeyote katika kizazi hiki kiovu na kisichomjali Mungu anayenionea aibu mimi na mafundisho yangu, Mwana wa Mtu atamwonea aibu mtu huyo wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu." Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE. Bible Hub |