1 Petro 4
Swahili NT
1Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi. 2Tangu sasa, basi, maisha yaliowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, si na tamaa za kibinadamu. 3Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu. 4Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni. 5Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu wazima na wafu! 6Kwa sababu hiyo, hao waliokufa ambao walikuwa wamehukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama anavyohukumiwa kila mmoja, walihubiriwa Habari Njema kusudi katika maisha yao ya kiroho waishi kama aishivyo Mungu.

7Mwisho wa vitu vyote umekaribia. Kwa hiyo mnapaswa kuwa na utaratibu na nidhamu, ili mweze kusali. 8Zaidi ya yote pendaneni kwa moyo wote, maana upendo hufunika dhambi nyingi. 9Muwe na ukarimu ninyi kwa ninyi bila kunung'unika. 10Kila mmoja anapaswa kutumia kipaji alichojaliwa na Mungu kwa faida ya wengine, kama vile uwakili mwema wa zawadi mbalimbali za Mungu. 11Anayesema kitu, maneno yake na yawe kama maneno ya Mungu; anayetumika anapaswa kutumikia kwa nguvu anayojaliwa na Mungu, ili katika mambo yote, Mungu atukuzwe kwa njia ya Yesu Kristo, ambaye utukufu na nguvu ni vyake milele na milele! Amina.

12Wapenzi wangu, msishangae kuhusu majaribio makali mnayopata kana kwamba mnapatwa na kitu kisicho cha kawaida. 13Ila furahini kwamba mnashiriki mateso ya Kristo ili mweze kuwa na furaha tele wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14Heri yenu ikiwa mnatukanwa kwa sababu ya jina la Kristo; jambo hilo lamaanisha kwamba Roho mtukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yetu. 15Asiwepo mtu yeyote miongoni mwenu ambaye anapaswa kuteseka kwa sababu ni muuaji, mwizi, mhalifu au mwovu. 16Lakini kama mtu akiteseka kwa sababu ni Mkristo, basi asione aibu, bali amtukuze Mungu, kwa sababu mtu huyo anaitwa kwa jina la Kristo. 17Wakati wa hukumu umefika, na hukumu hiyo inaanza na watu wake Mungu mwenyewe. Ikiwa hukumu hiyo inaanzia kwetu sisi, basi mwisho wake utakuwa namna gani kwa wale wasioamini Habari Njema ya Mungu? 18Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni vigumu kwa watu waadilifu kuokolewa; itakuwaje basi kwa wasiomcha Mungu na wenye dhambi?" 19Kwa hiyo, wale wanaoteseka kufuatana na matakwa ya Mungu, wanapaswa, kwa matendo yao mema, kujiweka chini ya Muumba wao ambaye ni wa kuaminika kabisa.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

1 Peter 3
Top of Page
Top of Page