Matayo 16
Swahili NT
1Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba afanye ishara itokayo mbinguni. 2Lakini Yesu akawajibu, "Wakati wa jioni ukifika ninyi husema: Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu! 3Na alfajiri mwasema: Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda! Basi, ninyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui. 4Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara yoyote isipokuwa tu ile ya Yona." Basi, akawaacha, akaenda zake.

5Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate. 6Yesu akawaambia, "Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!" 7Lakini wao wakawa wanajadiliana: "Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate." 8Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate? 9Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu elfu tano? Je, mlijaza vikapu vingapi vya makombo? 10Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu elfu nne, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki? 11Inawezekanaje hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!" 12Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

13Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?" 14Wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa ni Yohane mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii." 15Yesu akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?" 16Simoni Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai." 17Yesu akasema, "Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana si binadamu aliyekufunulia ukweli huu, ila Baba yangu aliye mbinguni. 18Nami nakwambia: wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala kifo chenyewe hakitaweza kulishinda. 19Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni." 20Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.

21Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake: "Ni lazima mimi niende Yerusalemu, na huko nikapate mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Nitauawa, na siku ya tatu nitafufuliwa." 22Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: "Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!" 23Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, "Ondoka mbele yangu Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya mungu bali ni ya kibinadamu!"

24Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza; 26lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake? 27Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.

28Kweli nawaambieni, wako wengine papahapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika Ufalme wake."



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 15
Top of Page
Top of Page