Matendo Ya Mitume 1
Swahili NT
1Ndugu Theofilo, Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake 2mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua. 3Kwa muda wa siku arobaini baada ya kifo chake aliwatokea mara nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai. Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu. 4Wakati walipokutana pamoja aliwaamuru hivi: "Msiondoke Yerusalemu, bali ngojeeni ile zawadi aliyoahidi Baba, zawadi ambayo mlikwisha nisikia nikiongea juu yake. 5Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache, ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu."

6Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, "Je Bwana, wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?" 7Lakini Yesu akawaambia, "Nyakati na majira ya mambo hayo viko chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini. 8Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni ninyi, mtajazwa nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia."

9Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena. 10Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao, 11wakasema, "Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni atakuja tena namna hiyohiyo mliivyomwona akienda mbinguni."

12Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko karibu kilomita moja kutoka mjini. 13Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na Yuda mwana wa Yakobo. 14Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.

15Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao, 16akasema, "Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi, alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu nguvuni. 17Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki huduma yetu. 18("Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo yake yakamwagika nje. 19Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba Hekeli Dama, maana yake, Shamba la Damu.)

20Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi: Nyumba yake ibaki mahame; mtu yeyote asiishi ndani yake. Tena imeandikwa: Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.

21Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa ufufuo wake Bwana Yesu. 22Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa kutoka kwetu kwenda mbinguni." 23Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia. 24Kisha wakasali: "Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo, utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua 25ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda mahali pake mwenyewe." 26Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

John 21
Top of Page
Top of Page