Yohana 8
Swahili NT
1lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni. 2Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha. 3Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao. 4Kisha wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. 5Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?" 6Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole. 7Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe." 8Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini. 9Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. 10Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?" 11Huyo mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu akamwambia, "Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena."

12Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima." 13Basi, Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali." 14Yesu akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda. 15Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu. 16Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami. 17Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali. 18Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia." 19Hapo wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia." 20Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.

21Yesu akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika." 22Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: Niendako ninyi hamwezi kufika?" 23Yesu akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. 24Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba Mimi ndimi, mtakufa katika dhambi zenu." 25Nao wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni tangu mwanzo! 26Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake." 27Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba. 28Basi, Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba Mimi ndimi, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha. 29Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza." 30Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.

31Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. 32Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru." 33Nao wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: mtakuwa huru?"

34Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi. 35Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. 36Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli. 37Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu. 38Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu."

39Wao wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu, 40Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo! 41Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu." 42Yesu akawaambia, "Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma. 43Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu. 44Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo. 45Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini. 46Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini? 47Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu."

48Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?" 49Yesu akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi hamniheshimu. 50Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu. 51Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele." 52Basi, Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele! 53Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?" 54Yesu akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza. 55Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na ninashika neno lake. 56Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi." 57Basi, Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?" 58Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko." 59Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

John 7
Top of Page
Top of Page