Luka 3
Swahili NT
1Mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alikuwa anatawala mkoa wa Yudea. Herode alikuwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, alikuwa mkuu wa mikoa ya Iturea na Trakoniti. Lusania alikuwa mkuu wa mkoa wa Abilene, 2na Anasi na Kayafa walikuwa makuhani wakuu mjini Yerusalem. Wakati huo ndipo neno la Mungu lilipomjia Yohane, mwana wa Zakariya, kule jangwani. 3Basi, Yohane akaenda katika sehemu zote zilizopakana na mto Yordani, akihubiri watu watubu na kubatizwa ili Mungu awaondolee dhambi.

4Ndivyo ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake; nyosheni mapito yake.

5Kila bonde litafukiwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa; palipopindika patanyooshwa, njia mbaya zitatengenezwa.

6Na, watu wote watauona wokovu utokao kwa Mungu."

7Basi, Yohane akawa anawaambia watu wengi waliofika ili awabatize: "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea kwamba mngeweza kuiepuka ghadhabu inayokuja? 8Basi, onyesheni kwa matendo kwamba mmetubu. Msianze sasa kusema: Sisi ni watoto wa Abrahamu. Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyageuza mawe haya yawe watoto wa Abrahamu! 9Lakini, sasa hivi shoka limewekwa tayari kukata mizizi ya miti. Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni."

10Umati wa watu ukamwuliza, "Tufanye nini basi?" 11Akawajibu, "Aliye na nguo mbili amgawie yule asiye na nguo; aliye na chakula afanye vivyo hivyo." 12Nao watoza ushuru wakaja pia ili wabatizwe, wakamwuliza, "Mwalimu, tufanye nini?" 13Naye akawaambia, "Msitoze ushuru zaidi ya kima kilichowekwa." 14Nao askari wakamwuliza, "Na sisi tufanye nini?" Naye akawajibu, "Msichukue vitu vya mtu yeyote kwa nguvu wala kumshtaki yeyote kwa uongo. Toshekeni na mishahara yenu."

15Wote walikuwa wanatazamia kitu fulani; basi, wakaanza kujiuliza mioyoni mwao kuhusu Yohane: kuwa labda yeye ndiye Kristo. 16Hapo Yohane akawaambia wote, "Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi ambaye sistahili hata kumfungulia kamba za viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 17Yeye ni kama mtu anayeshika mikononi mwake chombo cha kupuria nafaka, aipure nafaka yake, akusanye ngano ghalani mwake, na makapi ayachome kwa moto usiozimika."

18Hivyo, pamoja na mawaidha mengine mengi, Yohane aliwahimiza watu akiwahubiria Habari Njema. 19Lakini Yohane alimgombeza Herode, mkuu wa mkoa, kwa sababu alikuwa amemchukua Herodia, mke wa ndugu yake, na kumfanya mke wake; na pia kwa ajili ya mabaya yote aliyokuwa amefanya. 20Kisha Herode akazidisha ubaya wake kwa kumtia Yohane gerezani.

21Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa. Na alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka, 22na Roho Mtakatifu akamshukia akiwa na umbo kama la njiwa. Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe."

23Yesu alipoanza kazi yake hadharani, alikuwa na umri upatao miaka thelathini, na watu walidhani yeye ni mwana wa Yosefu, mwana wa Heli. 24Heli alikuwa mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, mwana wa Melki, mwana wa Yanai, mwana wa Yosefu, 25mwana wa Matathia, mwana wa Amosi, mwana wa Nahumu, mwana wa Hesli, mwana wa Nagai, 26mwana wa Maathi, mwana wa Matathia, mwana wa Shemeni, mwana wa Yoseki, mwana wa Yuda, 27mwana wa Yohanani, mwana wa Resa, mwana wa Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mwana wa Neri, 28mwana wa Melki, mwana wa Adi, mwana wa Kosamu, mwana wa Elmadamu, mwana wa Eri, 29mwana wa Yoshua, mwana wa Eliezeri, mwana wa Yorimu, mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, 30mwana wa Simeoni, mwana wa Yuda, mwana wa Yosefu, mwana wa Yonamu, mwana wa Eliakimu, 31mwana wa Melea, mwana wa Mena, mwana wa Matatha, mwana wa Nathani, mwana wa Daudi, 32mwana wa Yese, mwana wa Obedi, mwana wa Boazi, mwana wa Salmoni, mwana wa Nashoni, 33mwana wa Aminadabu, mwana wa Admini, mwana wa Arni, mwana wa Hesroni, mwana wa Feresi, mwana wa Yuda, 34mwana wa Yakobo, mwana wa Isaka, mwana wa Abrahamu, mwana wa Tera, mwana wa Nahori, 35mwana wa Serugi, mwana wa Reu, mwana wa Pelegi, mwana wa Eberi, mwana wa Sala, 36mwana wa Kainani, mwana wa Arfaksadi, mwana wa Shemu, mwana wa Noa, mwana wa Lameki, 37mwana wa Mathusala, mwana wa Henoki, mwana wa Yaredi, mwana wa Mahalaleli, mwana wa Kenani, 38mwana wa Enosi, mwana wa Sethi, mwana wa Adamu, aliyekuwa wa Mungu.



Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Luke 2
Top of Page
Top of Page