Marko 1
Swahili NT
1Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie; yeye atakutayarishia njia yako.

3Sauti ya mtu imesikika jangwani: Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni mapito yake."

4Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba ni lazima watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao. 5Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani. 6Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 7Naye alihubiri akisema, "Baada yangu anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. 8Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu."

9Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani. 10Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa. 11Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe."

12Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, 13akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamtumikia.

14Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, 15Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!

16Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu. 17Yesu akawaambia, "Nifuateni nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu." 18Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata. 19Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao. 20Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.

21Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika Sunagogi, akaanza kufundisha. 22Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka. 23Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu, 24akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!" 25Yesu akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu." 26Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka. 27Watu wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!" 28Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika wilaya ya Galilaya.

29Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao. 30Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili. 31Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.

32Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo. 33Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango. 34Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.

35Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali. 36Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta. 37Walipomwona wakamwambia, "Kila mtu anakutafuta." 38Yesu akawaambia, "Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo." 39Basi, akaenda kila mahali Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.

40Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba, "Ukitaka, waweza kunitakasa!" 41Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, "Nataka, takasika!" 42Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika. 43Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwonya vikali, 44Usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani; kisha utoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona. 45Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.Public Domain Swahili New Testament -- PLEASE MAKE COPIES FOR YOUR FRIENDS, NO ROYALTY DUE.

Bible Hub

Matthew 28
Top of Page
Top of Page